TAKRIBANI WALIMU WAPYA 28638 KUPELEKWA VIJIJINI.
![]() |
Naibu Waziri wa Elimu Philip Mulugo(kushoto) |
Mikoa hiyo ni ile ambayo inakabiliwa na changamoto ya uduni wa miundo mbinu, mazingira bora ya kufanyia kazi na kukosa motisha kwa wafanyakazi kama vile nyumba za kuishi.
Utaratibu huo wa ajira mpya hautahusisha majiji na manispaa ambako walimu wengi hukimbilia baada ya kupata ajira na serikali imepanga kuwachukulia hatua watumishi wake zaidi 800 waliotoroka kazini na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu bila idhini ya mwajiri.
Hatua hiyo ilitangazwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliyoitoa wakati akizungumza na wahitimu zaidi ya 700 wa Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo mkoani Iringa.
Mulugo alisema licha ya kuamua kuajiri walimu 28,638 idadi ya walimu wote waliohitimu kwenye vyuo vinavyotoa mafunzo hayo haikamilishi idadi hiyo.
“Wote hapa, tutawaajiri, lakini safari hii, hakuna ajira mijini na wote mtakaoajiriwa, tunawapeleka katika wilaya zenye changamoto, kwa hiyo mtakwenda mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Shinyanga, Manyara, Mtwara na Lindi. Tamko la serikali ndio hilo na mfahamu kabisa kwamba ajira hizi hazitahusu majiji na manispaa,” alisema Mulugo.
Alisema ajira hizo zitangazwa rasmi Januari mwaka 2013 huku akionya kuwa wahitimu hao wa shahada ya kwanza ya ualimu katika fani mbalimbali wasithubutu kuwashawishi maofisa waandamizi wa wizara kuomba kuteuliwa kuwa maofisa elimu wa wilaya na mikoa.
Kuhusu walimu waliotoroka kazini na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri, Mulugo alisema serikali imegundua kuwa tatizo hilo limeiathiri zaidi mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.
“Nawatangazia kiama wale ambao walitoroka kazini na kuja kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri wake…Wizara imewaagiza maofisa elimu wa Wilaya na Mikoa kuleta haraka majina hayo wizarani ili tuchukue hatua kali,” alisema Mulugo.
SOURCE:
Nipashe
November 19,2012.